Sunday, July 22, 2012

NAMNA YA KUOMBA

      - Hatua na vipengele muhimu katika kuomba -

MKARIBISHE ROHO MTAKATIFU. *Rum 8:26-27 *Yoh 14:16-17

Yesu alisema Roho Mtakatifu ni msaidizi wetu. Atatusaidia na kutufundisha yote, kwa maana pasipo yeye, sisi hatuwezi neno lolote. Na sisi peke yetu hatujui kuomba ipasavyo, bali yeye (Roho) ajua kutuombea kwa Mungu kama vile Mungu apendavyo. Hivyo kabla ya kuanza maombi au kusoma neno au ibada au safari au mitihani au kikao n.k. jifunze kujikabidhi kwa Roho Mtakatifu, uombe msaada wake, akupe ufanisi/ubora katika yote yakupasayo kufanya.

Tambua Utu wake, Uungu na Uweza wake.

Jikabidhi katika Nguvu ya Uongozi wake.

Tii kila Uongozi anaokupa.

FANYA TOBA NA UTAKASO. *Isa 59:1-2, Yoh 9:31, 1Yoh 1:8-9,7

Sikio la Bwana si zito kusikia wala mkono wake si mfupi kushindwa kututendea mambo tumwombayo, bali maovu yetu ndiyo yanatufarakanisha na Mungu wetu. Mungu hawasikii wenye dhambi. Hivyo chukua muda wa kutafakari na kuungama dhambi zako mbele za Mungu na kuzitubu kwa kumaanisha kuziacha. Mungu ni mwaminifu kutusamehe na kututakasa na uchafu wote. (Isa 1:18). Lakini, kabla hujafanya toba yako binfsi;

1. Kwanza, samehe wote waliokukosea, hata kama hawajaja
kukuomba msamaha. Usipowasamehe waliokukosea, na Mungu
hataweza kukusamehe wewe. (Math 6:12,14-15)
2. Ndipo nawe ufanye toba yako binafsi. Na Mungu atakusamehe kabisa.
Hata kama ni nyekundu sana, zitakuwa nyeupe sana. (Isa 1:18, Isa 43:25)

3. MSIFU, MUABUDU NA KUMSHUKURU MUNGU. *Zab 147 na Zab 148
Msifu Bwana kwa Matendo yake makuu, mwabudu Bwana kwa uzuri wake na kwa sifa zake. Mwadhimishe Mungu kwa Tabia zake, wema wake, fadhili zake na baraka zake mbalimbali anazotutendea. Sifa yako ikifika vizuri mbele za Mungu, ndipo atakuwa tayari kukupa haja za moyo wako. Haja zetu zimefichwa nyuma ya mgomgo wa sifa. Ndio maana Neno linasema;
‘Nawe utajifurahisha kwa Bwana (kwa kumsifu, kumwabudu na kumshukuru), naye atakupa
haja za moyo wako’ (Zab37:4).

Yesu anatuonyesha mfano; angalia sentensi yake ya kwanza katika kuomba kwake imekuwa “Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe.” (Math 6:9). Anaanza maombi kwa kumsifu Mungu. Msifu Mungu kwa kuimba na kwa kunena/kusema/kuelezea. Mungu anataka kusifiwa na kutukuzwa. Ukifanya sifa nzuri, ya kuufurahisha moyo wake, atakupa hata na vile ambavyo hukutegemea/hukuomba.

4. MWELEZE MUNGU MAHITAJI NA HOJA ZAKO. *Wafilipi 4:6-7,19 Isa 43:26
Mweleze Mungu zile hoja zilizokusukumwa kwenda kumwomba. Nenda mbele za Mungu kama ‘kuhani’ (1Pet 2:9). Kwa unyenyekevu na heshima. Lakini kabla ya kumweleza mahitaji yako binafsi;

(i) Kwanza fanya ‘maombezi’ – ombea watu wengine; (1Tim 2:1-4)

Viongozi mbalimbali na wenye mamlaka, watumishi wa Mungu, marafiki zako, wenye shida, ndugu zako, nchi yako, shule yako, shirika lenu, ofisi yenu, chama chenu, n.k. Usianze kujiombea mwenyewe tuu, zoea kuwatanguliza wengine.

(ii) Kisha fanya ‘maombi yako’– ombea haja za moyo wako. (Math 7:7-11)

Mweleze Mungu haja zako. Ongea na Mungu kwa uwazi na ukweli. Japo anazijua haja zetu, lakini ameagiza kuwa tumwombe ndipo atafanya.‘aombaye hupokea’ yaani; asiyeomba, hapati. Mungu anasema tumpelekee hoja zenye nguvu (Isa 41:21). Omba vitu vizuri na mambo makubwa ili upewe (pray for good things and big things)

5. FANYA MAOMBI YA VITA VYA ROHONI. *Efe 6:10-13 *2Kor 10:3-5

Baada ya kumwendea Mungu na kumweleza mahitaji yako, sasa simama kama ‘mfalme’, kwasababu wewe ni ‘mfalme’ (Ufu 5:8), tumia mamlaka yako ya kifalme, ongea na hali/hitaji ulilokuwa unaliombea, na kwa mamlaka, amuru iwe kama vile ulivyoomba/unavyotamani. Ndio maana Bwana Yesu alipokabidhiwa mamlaka yote na Mungu, naye akatukabidhi sisi (kanisa lake) “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za yule adui. Wala hakuna kitakachowadhuru” (Luk 10:19, Yer 1:10, Yak 4:7). Tuma neno lenye mamlaka katika hali/jambo ulilokuwa unaliombea, Amuru iwe vile ulivyokuwa unamwomba Mungu iwe. Kemea kila roho ya shetani inayoweza kuwa inasababisha tatizo katika swala lako.

6. OMBEA ULINZI JUU YA ULIYOYAOMBEA. *Math 6:13a

Baada ya kupiga vita vya kiroho, weka ulinzi katika yale uliyoyaombea, ili shetani na mapepo yake wasiweze kuirudia hali/jambo/mtu yule uliyemkomboa kwa maombi ya vita. Yesu alisema shetani akifukuzwa mahali, haendi mbali, anasubiri kuona kama atapata upenyo wa kuparudia mahali pale alipokuwa kwanza. (Math 12:43-45). Kwahiyo, usipoweka ulinzi, kuna uwezekano wa adui kurudi na kuliharibu zaidi lile jambo uliloliombea na kulipata.

Kumbuka, unapoomba vizuri, unapokea papo hapo (katika ulimwengu wa roho), lakini udhihirisho wake katika ulimwengu wa mwili, unaweza kuchukua muda fulani. Hivyo katika muda huo wa kusubiri, shetani anaweza akapita na kuzuia au kuharibu kile unachokisubiri kidhihirike katika ulimwengu wa mwili. Ndio maana Yesu alitufundisha kuombea ulinzi, “tuokoe na yule mwovu” (Math 6:13a). Weka ulinzi juu ya mambo yako yote. Jengea wigo wa moto wa mbinguni (2Fal 6:16-17), Yafunike kwa damu ya Yesu na agiza malaika walinzi walinde mambo yako masaa yote. Omba hivyo kila siku. (Zab 34:7, Zab 91:9-11, Ebr 1:13-14)

MSIFU, MWABUDU NA KUMSHUKURU MUNGU. *Math 6:13b

Yesu alianza maombi kwa kumsifu Mungu na kumtukuza. Na akamaliza maombi yake kwa kumtukuza Mungu tena. Akasema “kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu ni zako, sasa na hata milele” akamaliza. Kwahiyo nawe kwa kumaliza maombi yako, msifu na kumshukuru Mungu tena, kwa ukuu wake, uaminifu wake, na ahadi zake juu yetu.Ndipo ufunge maombi yako.

MUHIMU: TUMIA MAANDIKO KATIKA KUOMBA *Kol 3:16

-Katika kuomba kwako, mara zote tumia maandiko kumkumbusha Mungu ahadi zake .(Isa 43:26). Mungu analiangalia neno lake ili alitimize. Sababu pekee itakayomfanya Mungu akupe alichoomba, ni ili kulitimiza neno lake. Hivyo, baada ya kumweleza unachohitaji (kwa ajili yako au kwa ajili ya mtu unayemwombea) mpe Mungu andiko/neno lake linalokupa wewe uhalali wa kuomba hicho kitu mbele zake na kupewa.

-Hata unapompinga na kumkemea shetani, baada ya kutoa amri yako dhidi yake, shetani atasubiri kusikia andiko/neno linalomnyima yeye uhalali wa kushika alichoshika. Ndio maana Yesu alimshinda shetani kwa neno la Mungu. Alisema “imeandikwa” na shetani akashindwa. “Nao wakmshinda (shetani) kwa damu ya Yesu na kwa Neno” (Ufu 12:11)

MBINU ZA KUKUSAIDIA KUOMBA VIZURI KWA MUDA MREFU

1. CHAGUA MAHALI PAZURI PA UTULIVU. *Mk 1:35
ili uweze kuomba kwa utulivu na kwa umakini, chagua au tafuta mahali pazuri
patakapokupa utulivu katika kuomba (concentration in prayer). Ndio maana Mungu
alipenda kuongea na Musa juu ya mlima. (Kut 24:12-18). Hata Yesu alizoea kwenda
kuombea mlimani, mahali palipo mbali na vurugu za watu, alipenda kwenda mlimani.

(Math 14:22-23). Tafuta mahali patulivu; chumbani, kanisani, mlimani (Math 6:5-6)

2. CHAGUA MUDA MZURI. *Mhu 3:1,7
Ili uweze kuomba kwa umakini mzuri, chagua muda mzuri ambao akili yako ma mwili
wako viko fresh. Usilazimishe kuomba hata kama akili yako au mwili wako umechoka sana. Kila jambo lina wakati wake. Kama umechoka sana, huo si muda wa kuomba, bali wa kupumzika. Usilazimishe ratiba. ni bora upumzike ili baadaye uweze kuomba vizuri baadaye. Usije ukajikuta unamkemea Yesu badala shetani. Penda kuomba wakati una nguvu ya akili na mwili, ili uwe makini kuongea na Mungu kwa akili timamu. Ndio maana Yesu alipenda kuamka alfajiri sana kwenda kuomba mlimani. (Mk 1:35, Luka 4:42)

3. OMBA KATIKA ROHO (NENA KWA LUGHA). *Efe 6:18, Rum 8:26-27
Mbinu nyingine nzuri ya kuomba kwa muda mrefu na kwa ufanisi, ni kuomba kwa Roho; yaani kuomba kwa kunena kwa lugha. Tunapoomba kwa akili za kibinadamu, Mungu anasikia pia, lakini maombi yako yanakuwa na mipaka / limited kwasababu akili ya mtu haijui kila kitu. Bali Roho wa Mungu anajua kila kitu. Naye hutupa kipawa cha kuomba kwa lugha ya mbinguni iliyo bora zaidi.(Yuda 1:20, Mk 16:17, 1Kor 14:1-4, 15-16,7)

4. OMBA KWA KUFUNGA WAKATI MWINGINE. *Math 6:16-18
Kufunga kula kunasaidia kudhoofisha mwili, ili roho iwe makini zaidi kuongea na Mungu kwa kina zaidi. Mwili huu siku zote haupendi kufanya mambo ya Mungu. Na mwili ukiwa umeshiba, unakuwa na uchovu na uzito wa kufanya mambo ya kiroho. Mbinu mojawapo ya kuudhibiti, ni kuunyima/kuupunguzia posho yake ya chakula. Mwili ukidhoofika kiasi, roho yako inapata nguvu na upenyo mzuri zaidi (Zab 35:13). Mashujaa wote wa imani walifunga na kuomba. Ndio maana Yesu anasema ‘mfungapo’ akimaanisha ratiba ya kufunga, ipo. Inasaidia.

5. OMBA NA RAFIKI (PRAYER PARTNER). *Mhu 4:9-10
Neno la Mungu linasema, ni heri wawili kuliko mmoja. Kuna faida ya kuomba pamoja na rafiki yako. Kwanza, mnapokuwa wawili au watatu, inaleta hamasa na ari ya kuomba zaidi. Si rahisi kujisikia mvivu unapokuwa na waombaji wenzako. Pili; nguvu ya kiroho inaongezeka. Neno linasema, mwombaji mmoja anafukuza adui elfu moja, bali wakiwa wawili, wanafukuza (sio elfu mbili) bali elfu kumi! Shangaa! (Kumb 32:20) Hiyo ni kanuni ya mbinguni/kanuni ya Ki-Mungu. Kadri mnavyoongezeka, nguvu ya Mungu huongezeka.

Kwahiyo, wakati mwingine, omba na rafiki yako, unayemwamini, unayeweza kumshirikisha mambo yako ya binafsi. Mashujaa wengi wa imani, walikuwa na marafiki wa kiroho. (Prayer Partners). Kwa Mfano:- Math 17:1-9

Musa - alikuwa na Joshua, Haruni na Huri

Eliya - alikuwa na Elisha

Daniel - alikuwa na Shadrack, Meshack na Abednego.

Yesu - alikuwa na Petro, Yakobo na Yohana.

Paul - alikuwa na Barnaba, Timotheo na Tito.

Wewe Je? Uko na nani katika urafiki wa kiroho?Kama huna rafiki wa karibu wa kuomba naye, usikurupuke kujichagulia. Tulia umwombe Mungu akupe mtu atakayekuwa wa msaada kwako. Mtu mtakayefungamanishwa naye katika roho, hata kama mmetengana kijiografia, lakini katika roho, mko na umoja mzuri wa imani. (Math 18:18-19)

6. OMBA KATIKA MKAO UNAOKUPA UHURU NA NGUVU ZAIDI.

Katika kuomba kwa muda mrefu, mkao uliouzoea utakusaidia kwenda mwendo mrefu. Yakupasa kujua nguvu yako na udhaifu wako (strong point and weak point). Wakati wa kuomba, epuka mikao inayokuchosha haraka na tumia mikao inayokua nguvu zaidi. Kwa Mfano:- Ukiwa umechoka, usipende kuomba kwa kupiga magoti au kwa kuegemea kitandani. Ni bora uombe ukiwa umesimama au unatembea tembea, ili kuepuka usingizi na uchovu. Waombaji hodari wanaujua mikao inayowasaidia kuomba maombi marefu. Wengine hawana mikao maalum, bali wakiwa katika maombi, huwa wanabadilisha-badilisha mikao ili wasichoke. Hiyo ni mbinu nzuri pia.

Mifano ya Mashujaa wa imani;

Ibrahim – aliomba kwa kusimama (Mwa 18:22)

Daniel - aliomba kwa kupiga magoti (Dan 6:10)

Paul - aliomba kwa kupiga magoti (Efe 3:14)

Yesu - aliomba kwa kulala chini (Math 26:38-39)

Eliya - aliomba kwa kukaa chini na

kuweka kichwa kati ya miguu (1Fal 18:42)

Mimi - huwa napenda kuomba kwa kutembea tembea

Naweza kumaliza kilomita nyingi chumbani kwangu

Nikitembea huku nikiomba.

Wewe Je? Unaujua mkao wa nguvu? Kama hujui, Tafuta kujua.

OMBA NA MUZIKI LAINI KWA KUMWABUDU MUNGU.

Muziki wa kiroho, na wataratibu, unaweza kukutengenezea mazingira mazuri sana ya kuomba kwa muda mrefu. Muziki wa kuabudu, unavuta uwepo wa Mungu kwa namna ya pekee. Neno linasema, waimbaji na wanamuziki walipoimba na muziki ukapigwa, nao wakawa kama mtu mmoja, utukufu wa Mungu ukashuka na kulijaza lile hekalu hata makuhani hawakuweza tena kuhudumu (2Nyak 5:12-14). Kule mbinguni, kila malaika wa sifa, ana kinubi (zeze/gitaa). Elisha hakutoa unabii, mpaka mpiga kinubi alipopiga kwa ustadi, ndipo mkono wa Bwana (Roho wa Mungu) alipokija juu yake, naye akatabiri.

Najaribu kukuonyesha, kuna connection kati ya muziki wa kiroho na utukufu wa Mungu. Kwahiyo, ukiweza kuomba huku umeweka kanda au CD ya nyimbo za kiroho za taratibu, utapata (experience) hamasa ya kiroho (motivation) na utasikia una nguvu ya kuomba kwa muda mrefu. Kama unaweza, tengeneza kanda au CD maalum yenye nyimbo nzuri unazozipenda wewe, ili uwe unaipiga wakati wa maombi. Utajikuta unaweza kuomba kwa muda mrefu na kwa bubujiko zuri zaidi.Mwl. Mgisa Mtebe,Bsc Economics

Mzumbe University,+255 713 497 654

mgisamtebe@yahoo.com

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...