Sunday, July 15, 2012

Kuishi maisha ya Imani, Katika Ulimwengu Usioamini!


Kuishi maisha ya imani maana yake ni kuwa kwa kipindi chote cha maisha yetu hapa duniani, kwa kipindi chote cha uhai wetu, na kwa namna yoyote ile inayoashiria maisha kama kuongea kwetu, kutenda kwetu, kuwaza kwetu, kuenenda kwetu, kuvaa kwetu, kula kwetu, kuona kwetu, kukiri kwetu, kutoa na kupokea kwetu, kufanya kazi kwetu, lupigana kwetu, kushinda kwetu, kuomba kwetu na hata namna yote ile ya kuwajibika kwetu kwa watu wengine tunayafanya haya yote kwa imani.

Tunayafanya haya yote kwa uhakika kabisa, kwa kutokuwa na mashaka wala hofu, tunayafanya kama vile tumejua mwisho wake hata kama hatujayaona kwa macho yetu bado. Kama kuna mambo tunatarajia katika kuishi kwetu, basi kuishi kwa imani katika hayo tunayoyatarajia ni kuishi tukiwa na uhakika na udhihirisho ya kuwa hayo mambo yatatokea na kufanyika halisi maishani mwetu bila kujali changamoto zitokanazo na imani yetu katika mambo hayo.

Katika tafsiri ya kitabu cha Waebrania 11:1Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayoni bayana ya mambo yasiyoonekana”. Kwa lugha nyingine naweza kusema, imani ni udhihirisho wa mambo ninayoyatarajia kuyapata, mambo ninayotumaini kuyapata, mambo ninayotamani na kuwa na shauku nayo katika maisha yangu. Kwa hiyo naishi kwa namna inayodhihirisha na kuthibitisha kabisa kuwa kuna mambo ninayoyangojea hapo mbele.

Kama imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, hii inamaanisha kuwa ni muhimu sana kuyajua hayo mambo yatarajiwayo ni mambo gani kwasababu siwezi kuwa na imani na kitu nisichokijua. Kwa mfano, siwezi kuwa na imani kama Yesu Kristo atarudi tena wakati simjui Yesu mwenyewe wala jambo lolote kuhusu yeye, siwezi kusema nina imani Yesu ataniponya wakati hata sijawahi kusikia habari za Yesu na kwamba yeye ana uwezo wa kuponya. Hivyo ni lazima niwe nimesikia habari za jambo Fulani, ni lazima niwe nimeyajua hayo mambo ninayoyatarajia ili niseme sasa nina imani nayo kwamba yatatokea kwangu.

Ninachosema hapa ni hiki, kwa sababu imani chanzo chake ni kusikia, ni muhimu sana kujua unasikia juu ya nini. Kila mtu hujenga imani ya kile anachokisikia na zaidi sana kile achokifahamu na kukijua. Ukisikia sana habari za waganga basi utajenga imani yako kwa waganga lakini kitu cha kujua hapa ni kuwa kama wewe ni raia wa ufalme wa Mungu basi ni lazima imani yako iwe katika mambo yatokanayo na ufalme huo.

Neno la Kristo ndio msingi wa kujenga imani ya kweli kwa kila aaminiye kwa moyo wake na kukiri kwa kinywa chake kwamba Yesu ni Bwana. Kwa hiyo kama nimeamua kuishi maisha ya imani ndani ya Yesu, ni lazima nizidi kumsikia sana Yesu ili nizidi sana kujenga imani yangu kwake kwenye mambo ninayotarajia.

Kabla sijajua kuwa Yesu ni mwokozi nilimdharau na kuwakejeli wote walionambia habari zake, kwa hiyo nisingeweza kuishi maisha ya imani wakati huo.

Nilipomjua Yesu ni nani, kwa kusikia, nikajenga imani yangu na kuanza kutarajia mambo kadha wa kadha yaliyondani yake yeye. Kwa hiyo hakika ya mambo yatarajiwayo inakuja kwa kuzidi sana kuongeza ufahamu katika kuyajua hayo mambo yaliyofungwa ndani yake yeye ninayemwamini.

Mambo yatarajiwayo, kwa tafsiri niliyoiweka hapo juu, inamaanisha mambo ninayotumainia ndani ya imani yangu katika Kristo na haya mambo ni kama:

  • Uzima

  • Uponyaji

  • Baraka za mwilini na za rohoni

  • Mafanikio na maendeleo

  • Maisha ya ushindi

  • Ulinzi

  • Uzima wa milele

  • Masomo

  • Chakula

  • Mavazi

  • Nguvu

Kwa kuchukua mfano mmoja hapo juu, mimi nimeokoka ingawa nimekuwa naishi maisha ya hali ya chini kiasi kwamba hata mahitaji ya msingi kama chakula, mavazi na hata mahali pa kulala sina, kuishi maisha ya imani katika hali hii ni kuwa na hakika juu ya hayo mambo ninayoyahitaji kuwa nitayapata kutegemeana na imani yangu katika yeye ninayeamini, yaani Kristo, kuwa anaweza kunipa hayo yote sawa sawa nay ale ninayoyafahamu na kuyajua, yale niliyoyasikia amesema kuwa atanifanyia.

Ingawa mwili wangu utaonekana kuchakaa lakini imani yangu inanipa nguvu na tumanini kwani ninajua kabisa kuwa ipo siku Yule ninayemwamini atayabadilisha maisha yangu kwa kadri ya imani yangu, kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yangu na zaidi sana kwa kadri ya utajiri wa utukufu wake.

Kwa upande mwingine, kuna mambo yasioonekana ambayo nayo tunatakiwa tuishi kana kwamba tumeyaona na hapa Neno la Mungu linasema, Imani ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Neno bayana ni sawa na kusema halisia, imani ni uhalisia, waziwazi au inayooneka kabisa kwa macho ya nyama na damu. Umesubiria mtoto kwa muda mrefu, imani inakupa nguvu na tumaini la kuendelea kuishi maisha yako kila siku kama mama aliyepata mtoto tayari. Bayana.

Halisia. Inayoonekana. Kama kuna jambo lolote lile ninalolingojea na bado sijaliona, ninatakiwa niwe nalingojea kama vile nimeshaliona kama vile Babu Ibrahimu, habari zake zinasema alitarajia yasiyoweza kutarajia, alitarajia mambo yasiyoonekana kana kwamba yameonekana, alimtarajia Isaka wakati hali yake na ya Bibi Sara haikuwa na uwezo wa kuwapa motto.Lakini yeye alisubiri katika kutarajia kwake mambo yasiyoweza kutarajiwa kabisa. Nguvu ya imani yake aliipata kwa kumjua anayemwamini.

“Mjue sana Mungu, ili uwe na amani na ndivyo mema yatakavokujia”, ndivyo utakavyozidi kupata ushindi maishani mwako, ndivyo utakavyozidi kushinda vita na makwazo ya duniani hapa na ndivyo utakavyozidi kuishi maisha yenye utulivu na usalama kwa maana unamjua yeye akupaye nguvu za hata kupata utajiri.

Kwa hiyo kuishi maisha ya imani ni katika hali zote kwa maana pasipo hiyo imani haiwezekani kabisa kumpendeza Mungu kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima, sio ombi, lazima aamini (awe na hakika wa mambo anayotarajia toka kwake) kwamba yeye Mungu yuko na zaidi ya hayo huwapa thawabu, huwapa Baraka, huwapa mambo mema, huwapa mafanikio, huwapa hazina njema wale wote wanaomtafuta. Katika hali zote, kufanikiwa au kutokufanikiwa, kupata au kukosa, raha au mateso.

Imani inahitajika na hivyo wakati wa Furaha wewe furahi kwa imani na wakati wa majaribu ya imani yako usiseme hii sio imani kwani ni vema

kuhesabu ya kuwa ni Furaha tupu tunapoingia katika majaribu mbali mbali tukijua kuwa kujaribiwa kwa imani yetu huleta saburi maishani mwetu. Kwa hiyo neno imani lina maneno matano ambayo ni:

  1. Hakika-kutokuwa na shaka wala hafu, thabiti

  2. Mambo-ahadi za Mungu unazozijua kama Neno lake linavyosema

  3. Yatarajiwayo-tumaini la kungojea na kusubiri

  4. Bayana-halisia, inayoonekana

  5. Yasiyoonekana-kwa macho ya nyama na damu

Kwa hiyo, ninapomalizia ukurasa huu, napenda kusema kuwa kuishi maisha ya imani ni kuishi maisha tegemezi katika kile anachokisema Mungu. Ni kuishi maisha ya mtu wa haki, mwenye haki anaishi kwa imani, anaishi kwa kuwa na ujasiri na uhakika wa mambo yote anayoyatarajia hata kama hajayaona kwa macho yake. Tunawaza kwa imani, tunaongea kwa imani, tunakula kwa imani, tunatembea kwa imani, tunafanya kazi kwa imani, tunaomba kwa imani, tunaangaliakwa imani, tunaenenda kwa imani na kwa ujumla wake yote tunayoyafanya iwe ni kwa neno au kwa tendo tunayafanya yote kwa imani katika jina la Yesu tukizidi sana kumshukuru Mungu Baba.

Kwa maana tunajua ya kuwa pasipo imani, haiwezekani kumpendeza Mungu kwani sisi kama wenye haki imetupasa kuishi kwa imani. Kuna uhusiano kati ya kuwa mwenye haki na kuishi maisha ya imani. Haiwezekani mtu akaishi kwa imani bila kuhesabiwa haki katika Yesu Kristo aliye mwanzilishi wa imani yetu. Na huu uhusiano ndio tutakao uchambua na kujifunza juu ya kwa nini mwenye haki aishi kwa imani. Umebarikiwa katika jina la Yesu Kristo!

–Sehemu ya kitabu cha Mtumishi wa Mungu, Mwinjilisti Raphael Joachim Lyela

Mawasiliano zaidi kuhusu kitabu chake wasiliana nae
Email: annointedkaka@yahoo.com
Simu: 0787 110 003

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...